Vijana waishio mtaani na mitandao ya kijamii kaskazini mwa Tanzania

This is a Swahili translation of the presentation that I made at the RGS-IBG post-graduate conference in March earlier this year. To read this blog in English, please follow this link. I am extremely grateful to the following translators who poured over my presentation and devoted a significant amount of time understanding the meaning of my research and how to translate this best for a Swahili audience: Lucy Mariki, Asimwe Suedi and Devotha Festo Mlay. Unfortunately my Kiswahili isn't good enough to vouch for every word of this translation. So please forgive us where meanings and sentiments have been unintentionally misinterpreted.

---

Ijumaa iliyopita nilifanya uwasilishaji katika kongamano la nusu muhula la astashahada la RGS-IBG. Ilipendeza kuona mawasilisho tofauti kutoka katika nyanja mbalimbali za Jiografia. Nilirudi nyumbani na mitazamo ya kuvutia ya tafiti kutoka nyanja mbalimbali kuhusu chakula, dansi na ndoto ya Cecil Rhodes kuhusu mahusiano ya kisiasa kati ya nchi na nchi na miongoni mwa kundi moja la nchi na kundi jingine. Wawakilishiwa mkutano walishirikiana vizuri na watoa mada na mazingira ya kongamano yalikua rafiki.

Moja ya changamoto za kongamano lile ni kwamba vipindi vingi vya muhimu vilifanyika kwa wakati mmoja, hivyo haikuwezekana kuhudhuria vipindi na mawasilisho yote yaliyokuvutia. Kwa sababu hii, nimechapisha makala kutoka katika uwasilishaji wangu kama ifuatavyo. Ninaadhimia kufanya makala hii mjadala huru/wa wazi hivyo kama una swali la kuongezea hapo chini, tafadhali jisikie huru kuandika katika sanduku la maoni.


UTANGULIZI

Utafiti wangu unachunguza maisha na mahusiano ya watoto wanaoishi mtaani kaskazini mwa Tanzania kwa kutumia mbinu ya kuchanganua data ili kuunda nadharia“grounded theory”. Ninashirikiana na shirika la misaada la Uingereza linaloitwa StreetInvest, almaarufu kama “detached youth workers” linalowafundisha maafisa wa ustawi wa jamii kusikiliza kwa umakini, kuwaelewa na kuwasaidia watoto wanaoishi mtaani. Utafiti wangu ulikusudia kuelewa nafasi ya mahusiano katika maisha ya watoto waishio mtaani, na jinsi gani mahusiano ya afisa jamii huhusika katika mtandao huu mpana wa mahusiano.

MBINU NA HISTORIA

Nilitembelea eneo la utafiti mara mbili na nilitumia miezi 8 kufanya mahojiano. Nilifanya mahojiano na watu binafsi 25, mahojiano ya kikundi ambayo yalijumuisha watoto waishio mtaani na vijana wadogo 55, watu wazima ambao waliishi mtaani wakiwa watoto, wanajamii na wataalamu. Nilifanya utafiti huu kwa kutumia mchakato wa kuongeza na kupunguza. Kutathimini kwa kifupi kila mahojiano kabla ya kuandaa maswali ya mahojiano yanayofuata. Dhumuni la mbinu ya kuchanganua data ili kuunda nadharia (Grounded theory) si kukusanya data ili kujenga matokeo ambayo yanawakilisha idadi ya watu wote, bali kujenga nadharia kupitia mzunguko wa sampuli za kinadharia na uhifadhi wa mawazo ya kila data kwa wakati mmoja. Baada ya uchanganuzi kufanyika na makundi kupatikana, alama za kinadharia hutumika kuelewa uhusiano uliopo katika maudhui yaliyojitokeza kwenye data.

Mahojiano yalifanyika kwa watoto na vijana ambao hujulikana kama watoto wanaoishi mtaani waliokuwa na umri kati ya miaka 11 na 23, umri wa wastani ni miaka 17. Hatahivyo, ni vema kujua kwamba, ni vigumu kutambua umri sahihi katika eneo hili hivyo umri tajwa hapa uchukuliwe kama kiashiria na sio umri halisi. Pia, tulifanya mahojiano na wanajamii, watu wazima ambao waliwahi kuishi mtaani na wataalamu ambao hufanya kazi na watoto waishio mitaani.

Mara nyingi, mahojiano na watoto yalifanyika nyakati za jioni kwa kutumia kinakili sauti na maswali ya wazi yaliyojikita katika mada kuu (semi-structured questions). Watafiti wasaidizi walifundishwa kusikiliza kwa umakini na maswali wazi, na waliambiwa kuwa kipaumbele ni kumfanya mtoto ajisikie amesikilizwa, pia watafute kuelewa watoto wanachokisema badala ya kusisitiza kufuata mtiririko wa maswali. Tuliwanunulia washiriki wa mahojiano chakula cha jioni kama shukrani kwa ushiriki wao katika mahojiano.

Katika sampuli yetu, kulikuwa na msichana mmoja tu aliyehusishwa na maisha ya mtaani, na alirudi kwa bibi yake jioni. Mbali na huyu, hatukuwahi kukutana na msichana anayeishi mtaani. Tafiti kutoka nchi nyingine zinahusisha wasichana kuishi mtaani, hivyo kukosekana kwa wasichana katika eneo husika la utafiti huweza kuhusishwa na mitizamo ya kitamaduni juu ya wasichana. Baadhi ya washiriki walituambia kama wasichana wakitaka kuondoka nyumbani, mara nyingi huolewa au huishia kufanya kazi za ndani.

MJADALA WA DATA NA UCHANGANUZI

Matokeo yangu ya hivi sasa yanajikita katika makundi 13 tofauti. Ni mapema sana kwenye uchanganuzi wangu kuweza kufikia hitimisho halisi. Hatahivyo, nitapenda kujikita katika matokeo ya awali kuhusu mahusiano kwa ajili ya makala hii. Kipengele hiki kitaorodhesha vyanzo vitatu tofauti vya mahusiano ambavyo watoto wanaoishi mtaani na vijana wadogo waliyarejelea kipindi cha mahojiano. Vyanzo hivi ni makundi rika, wanajamii na mashirika yasio ya kiserikali.

Ili uweze kuishi mtaani, hapa kama mtoto au kijana mdogo aishie mtaani, unategemewa kuwa na uwezo wa kujenga mtandao wa mahusiano tofauti tofauti yenye nia fulani. Watoto waliripoti na tulishuhudia watoto wakitengeneza mahusiano ya mawanda mapana kipindi chote walipokuwa mtaani, na mahusiano haya yalikidhi haja/dhima mbalimbali.

KWANZA, KUNDI RIKA

Kupitia makundi rika, watoto waishio mtaani waliweza kushirikiana katika kutafuta kazi au kujifurahisha/kujiburudisha. Kundi rika pia walitumika kama kundi saidizi, kwani waligawana chakula au pesa pale ambapo mmoja wa watoto hakupata pesa kabisa au alipoumwa. Kwa mfano, kulikuwa na vielelezi vya uaminifu na maelewano kati ya watoto waliokuwa wakiishi mtaani.

“Ninachokitafuta kutoka kwa marafiki zangu ni kukaa nao na wao ni ndugu zangu kwasababu ninapopata tatizo mtaani wao ni wa kwanza kufahamu. (Ii.1, Mvulana, Miaka 18)

Hatahivyo, baadhi ya makundi rika huweza kuwa chanzo cha hatari. Kama mmojawao alidhaniwa kufanya uhalifu, kuna uwezekano wa polisi kuwakamata wote badala ya yule aliyehusika tu. Watoto wenye umri mdogo waliwalalamikia vijana wenye umri mkubwa kuwa walikuwa wakiwaibia na pia kuwatumia katika kuiba, kwani watoto wenye umri mdogo huonekana kutokuwa tishio sana. Japokuwa kuna uwezekano mkubwa wa watoto hawa wenye umri mdogo kulipwa kushiriki katika kazi hizi za uhalifu, bado iliwaweka katika hatari. Baadhi ya watoto walizungumzia namna marafiki wanavyoshauriana kutumia aina mpya za madawa ya kulevya na kama rafiki ataanza kujenga tabia mbaya ya kutumia madawa kama kokeini na heroini, watoto wanaweza kuvunja urafiki wao ili kujizuia kutumbukia katika utumiaji wa madawa hayo.

Kwa kifupi, watoto waishio mtaani wanategemea wenzao wa kundi rika kwa kampani ya kila siku na kimbilio la kwanza pale wanapohitaji msaada. Wana utambulisho na umoja, na hulinda maslahi ya kila mmoja wa kundi hili. Hatahivyo, wakati mwingine, watoto wenye umri mkubwa huwatumia watoto wenye umri mdogo, na baadhi ya watoto huchagua kuwaepuka watu wanaowafikiria kuwa na ushawishi mbaya.

PILI, WANAJAMII

Wanajamii wanaweza kuchagua kujitolea kumsaidia mtoto aishie mtaani kwa sababu nyingi/mbalimbali. Baadhi wanaweza kumfahamu mtoto baada ya muda fulani na kumchukua katika familia zao au kumpa kazi ya kufanya. Baadhi ya wamiliki wa maduka huwaruhusu watoto kulala kwenye veranda za maduka yao na kulikuwako na baadhi ya maeneo ambayo hugawa chakula au kuonesha sinema/video ambapo watoto waliruhusiwa kukaa bure au kwa gharama nafuu. Maeneo haya yamekuwa ni muhimu kwa usalama na hujulikana kwa watoto walioshiriki katika utafiti huu. Mara nyingi, wanawake wanaofanya kazi sokoni waliwapa watoto pesa au chakula kama ujira kwa kuwatuma, kuwasaidia kuchunga mizigo yao au kuwachotea maji. Watoto pia waliwauzia wanawake hawa vitu walivyovipata na kuufanya uhusiano wao kuwa wa manufaa kwa pande zote mbili.

Afisa ustawi wa jamii alieza“Ndio, wapo karibu sana (watoto na wanawake wafanyao kazi sokoni) kwasababu, unajua chakula ni kitu kinachomfanya kila mtu aishi hivyo ni rahisi kwao kuwa na uhusihano mzuri” (Afisa ustawi wa jamii, mwanamume)

Tulishuhudia watoto wakitaniana na kuongea kwa uhuru na baadhi ya wanawake sokoni hapo, ambao haikuwashangaza kuwaona watoto wakitumia muda mwingi kwa siku sokoni.

Hatahivyo, watoto na vijana huweza kufanyiwa ukatili na wanajamii. Watoto na vijana waishio mtaani hupata matusi na kuhisiwa vibaya na wanajamii ambao hawawafahamu. Kuna sababu nyingi zinazowasababisha wanajamii kuwapinga watoto na vijana waishio mtaani; moja ya sababu hizo ni kwamba, watoto na vijana waishio mtaani hudhaniwa kuwa wezi na wahalifu.Hiki, si lazima kiwe kiashiria kisicho cha haki kwani, watoto na vijana wanakiri kuiba ili wapate pesa, lakini wengi husema wanafanya vitendo hivi kwa kujuta.Pili, watoto na vijana waishio mtaani huoekana wakijishughulisha na mambo yanayochukuliwa kuwa si sahihi kwa umri wao, kama vile uvutaji wa sigara(Tazama mjadala wa status offense) na tatu, hisia kali huibuliwa na watoto waishio mtaani na vijana wanaoishi mbali na familia zao. Hoja hii ya tatu ilirejelewa sana kwenye mahojiano na kwenye maandiko kadhaa (Hollos 2002) yameonesha umuhimu wa majukumu ya famiia katika jamii za kitanzania.Kulingana na mtazamo wa mtazamaji kwenye maisha ya familia, watoto huonekana kama wametelekeza familia zao na hawatimizi majukumu yao ya kuzitunza familia zao. Watoto huchukuliwa kama watundu au wakorofi ambao hutoroka kazi ngumu na adhabu –adhabu ikichukuliwa kama kitangulizi cha kuja kuwa raia mwema. (Frankenberg et al,2010)

Kijana mmoja mdogo alituambia haya kwenye mada ya kupata kazi “Wanapokuona pia inakuwa vigumu kukupa kazi kwani hujiuliza ni kitu gani kimefanya uhusiano kati yako na wazazi wako kuharibika, ni kitu gani, nitawezaje kumuajiri wakati mama yake hana muda naye”. (l7;I, umri 22, mvulana)

Kwa kifupi, wakati kuna watu wengi katika jamii ambao huwatendea mema watoto waishio mtaani, mwitiko wa kusikitisha kutoka katika mahojiano ni kwamba watoto waishio mtaani hawaaminiki na wananyanyapaliwa hii huathiri ujasiri binafsi na hisia ya thamani ya utu wao lakini pia hufanya vigumu kwa watoto na vijana wadogo katika soko la ajira.

TATU NA MWISHO, MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI.

Watoto wengi waishio mtaani hujenga mahusiano au hujiusisha na huduma zinaotolewa na mashirika yasio ya kiserikali wakati fulani. Mahusiano waliyonayo na mashirika yasiyo ya kiserikali hutofautiana kutegemea na aina ya huduma wanayokua wanajihusisha nayo. Baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikakali hujulikana kama mahali ambapo watoto na vijana wadogo huweza kwenda kupata chakula, dawa na msaada endapo wataingia mikononi mwa polisi kwa tuhuma za uhalifu.Watoto na vijana waliongelea pia jinsi wanavyothamini maafisa ustawi wa jamii, na hata watafiti wanavyokuja kuwasikiliza na kuwapa ushauri kuhusu vitu sahihi vya kufanya. Baadhi ya watoto waliongelea jinsi wanavyokosa ushauri wa watu wazima au mtu wa kuwashauri njia sahihi wanazopaswa kuzifuata katika maisha.

Hatahivyo, wakati huu, vipaumbele vya mashirika yasio ya kiserikali haviungi mkono watoto waishio mtaani. Hii inaeza kuwa inasababishwa na baadhi ya mashirika haya kutokuchukua muda kuwaelewa watoto na vijana na vitu wanavyovipenda. Au, inawezakuwa kwasababu mashirika yasiyo ya kiserikali mara nyingi hufikiria viwango tofauti vya muda kuliko watoto na vijana wanavyofikiria. Mashirika mengi katika ukanda huu hufanya kazi na watoto wasiozidi miaka 15. Wakati wa utafiti tuligundua kuwa kadiri mtoto anavyokua, anakuwa vizuri katika kufikiria maisha yake ya mbeleni na wanakuwa na hamasa ya kupanga mipango ya baadaye ya kimafanikio. Watoto wanapokuwa wadogo, umri lengwa wa mashirika yasiyo ya kiserikali, wanakuwa wanafikiria sana kujikita katika mahitaji ya haraka kama chakula, mavazi, starehe na madawa na huwa hawana nafasi kubwa ya kuona au kuamini faida za kwenda shule au kutii sheria ili waweze kukaa kwenye makazi.

Mmoja wa afisa ustawi wa jamii alituambia: 

“Wanajifanya wanataka kwenda shule lakini ukweli ni kwamba, si kuwa wanataka kwenda shule, wana malengo yao kwamba tunamtumia mtu huyu kupata kile tunachokitaka. Hivyo wanajua shule ni mbinu ya kuweza kuishi, wanafahamu kuwa mtu huyu ana pesa kwasababu hiyo nitakuwa karibu naye na pale pesa zitakapoisha nitapita njia nyingine. (Afisa ustawi wa jamii mwanamume)

Watoto wakubwa na vijana tu ndio waliokuwa wakielewa madhara ya kukulia mtaani bila elimu.

Kijana mdogo mmoja alituambia”ukiwaangalia unadhani kuwa wanapaswa kuwa shuleni lakini wanakusanya vyuma chakavu” (li.2, miaka 17, mwnaume)

Watoto wakubwa na vijana, walionekana kujali/kukubali kupokea muongozo, msaada na mafunzo ya kutafuta ajira na walioneshwa kuhuzunishwa kwakuwa hawakuweza kupata msaada kutoka mashirika yasiyo ya serikali kwani umri wao ulikuwa mkubwa.

Kwa ufupi, watoto na vijana waishio mtaani wana mchanganyiko wa mahusiano na mashirika yasiyo ya kiserikali na huduma zake. Kwa namna moja, hutumia mashirika yasiyo ya kiserikali kuwasaidia kupata mahitaji ya haraka, ila hujikuta wakipatania uhuru wao wa kubaki mtaani kwani mashirika mengi yasiyo ya kiserikali hutia kipaumbele katika kuwaondoa watoto mtaani. Upande mwingine, watoto wakubwa hujutia nafasi walizozikosa walipokuwa wadogo na kuanza kutambua faida za kujitoa kikamilifu kujihusisha na elimu na huduma za mafunzo.

HITIMISHO

Katika hatua hii, ni mapema mno katika tathimini yangu kuhitimisha. Kujenga mtandao saidizi mtaani ni namna moja ambayo watoto na vijana wadogo huchukua jukumu wanapokutana na majanga ili kupata njia ya usalama na kujikimu.Vijana wadogo na watoto wanaweza kutiwa moyo na kusaidiwa katika njia hii, kwa kuongeza idadi ya watu wanaowatembelea mtaani, kuwasikiliza na kuwapa ushauri. Kwa watoto wadogo, itakua muhimu kuweka jitihada za muhimu katika kuwaongoza kwenye mchakato wa kufikiria maisha yao ya mbele na maisha ya mtaani yatawapeleka wapi. Kwa vijana wakubwa, ambao huchukuliwa kama kundi gumu kujihusisha nalo, kuna mawanda mapana kutumia hofu yao juu ya maisha yao ya mbeleni, kuwapa fursa ya kupata nafasi ya kupita katika njia za uhakika za maisha. Juhudi kama hizo huhitaji muda, uvumilivu na ubunifu. Maafisa ustawi wa jamii, na mashirika yasiyo ya kiserikali wana idadi kubwa ya visa vya wakati waliposaidia watoto na baadae huwakuta wamerudi tena mtaani. Ni muhimu kukumbuka kwamba watoto hawa na vijana wadogo mara nyingi hujitenga na hufanya maamuzi kupata mahitaji yao ya haraka.

Hatahivyo, hakuna mtoto anayetamani kuwa mtu mzima anayeishi mtaani, hivyo ni muhimu juhudi za mashirika yasiyo ya serikali ziwasaidie watoto kufikiria nje ya mahitaji yao ya haraka na kufanyia kazi malengo yao ya muda mrefu kwa umakini.

*Nilielezea jinsi gani si ukosefu wa elimu tu unaowazuia vijana kupata kazi, lakini pia ni matokeo ya kutokuwa na uwezo wa kuongeza mkusanyiko wa mapato. “kwa mfano, Kijana mdogo mmoja alifundishwa upishi, lakini hakuweza kutumia ujuzi huu kama namna ya kujipatia kipato cha kujikimu kwani hakuwa na nafasi/mahali pa kuweka sufuria zake wala sare za kumuwezesha kufanya kazi ya upishi. Hata kama angepata pesa za kutosha kununua sufuria, kukosekana kwa eneo la kuhifadhi sufuria hizo hufanya ununuzi wake kutokuwa na maana. Hivyo, changamoto ya watu hawa hujumuisha ujuzi na vitendea kazi.

**Pia nilizungumzia kwa kifupi jinsi watoto wanavyojulikana kwa kuweka akiba ya pesa kwa wanawake wa sokoni au wauza maduka na kuzitumia wakati wakiumwa au wakishindwa kufanya kazi, kununua nguo mpya kwaajili ya Krisimasi na Iddi, au huzitumia wakati wanajipa muda wa kutokufanya kazi kwa kipindi fulani. Hii inaonesha watoto wana mpango wa kujitosheleza wenyewe endapo kutakuwa na dharura kwa muda mfupi.

WAWAKILISHI WALIUZA MASWALI YAFUATAYO

Swali: Vipi kuhusu umuhimu wa uhuru kwa watoto waishio mtaani?

Jibu: Ndio, Hakika hii ni muhimu sana kwa watoto wengi na vijana wadogo tuliozungumza nao. Hiki ni kitu wanachokitaka kwa hakika, na mara walipopata uhuru, waliona vigumu kuupoteza tena. Ila ninatoa hoja kwamba kuna faida zinazopatikana kwenye mashirika na kujenga mahusiano ya kuaminika ambayo humaanisha kwamba wanahitaji kuchukua majukumu ya vitendo vyao na kuachia uhuru kidogo ambao huweza kuwa mzuri kwao. Tamaa yao ya kuwa huru ni kitu ambacho kinatakiwa kiheshimiwe lakini pia kipingwe.

Swali: Baadhi ya vitabu vinaongelea kuhusu marafiki wa mtaani kuchukua nafasi ya familia, je unaliona hili katika data zako?

Jibu: Nimeliona hili pia na kihalisia, baadhi ya maeneo ulimwenguni kuna familia nyingi za baba mama na watoto ambao huishi mitaani. Katika utafiti wangu, sidhani kama watoto wanawachukulia marafiki zao kama mbadala wa familia,. Walikuwa karibu sana na marafiki zao na walitunzana, lakini naweza kutoa hoja kwamba katika jamii ya mfumo dume, ukoo ni muhimu sana, hivyo marafiki hawawezi kuchukuliwa kuwa mbadala wa familia katika akili zao.

Kwa kuongezea, ingawa watoto walitegemeana na kusaidiana, bado walifanya maamuzi kwa kutegemea mahitaji yao ya msingi. Hivyo, kwa mfano, kama walifikiri kuondoka kwenda mji mwingine ni kitu ambacho kingewasaidia kupata pesa, waliongelea jinsi gani wangeondoka bila kufikiri sana kuhusu marafiki zao waliowaacha nyuma. Hivyo walikuwa na umoja sana lakini pia walikuwa na maamuzi binafsi.

Swali: Unafasili vipi mtoto aishiye mtaani?

Jibu: Kuna maana nyingi, na watafiti wengi wamejumuisha watoto wanaofanya kazi mtaani na kurudi nyumbani kwa wazazi/familia zao jioni. Watoto wa namna hii walikuwapo katika eneo langu la utafiti, lakini watoto tuliofanya mahojiano nao hawakuwajumuisha hawa kama watoto waishio mtaani. Ili uwe mtoto anayeishi mtaani kwa mtizamo wao ilikuwa ni kuishi, kufanya kazi na kulala mtaani, au uwe umefanya haya kipindi fulani huko nyuma. Hawa ni watoto au vijana wadogo ambao tuliweza kukutana nao sana tulipokuwa tukifanya utafitijioni.

Swali: Kuna namna yoyote ya kupinga unyanyapaa wanaoupata watoto wanaoishi mtaani?

Hii ni changamoto haswa. Mshirika wangu wa shirika lisilo la kiserikali pia huendesha mafunzo kwa polisi ili kupinga baadhi ya mitazamo hasi waliyonayo dhidi ya watoto waishio mtaani. Kijana mmoja mdogo tuliyekutana naye alijitahidi sana kupinga mtazamo huu kwa mienendo yake, alikuwa wa kuaminika, akitafuta kazi ndogondogo na kujenga uaminifu kwa watu wa sokoni baada ya muda na kuunda mkokoteni wa kuuzia matunda ili auze machungwa kandokando ya barabara. Alituambia “Nilitaka kulifuta jina la mtoto aishiye mtaani, na sasa siwezi kukosa kazi.” Kweli, bado kuna kazi kubwa ya kufanya kwani unyanyapaa umetopea sana, hata kama ilivyo katika nchi hii dhidi ya watu wasio na makazi.

Banner image taken from: https://cyclestyleboston.wordpress.com/2013/08/14/summer-abroad-moshi-tanzania/